Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amewakumbusha vijana wenye uelewa kuhusu mazingira kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa vijijini wasio na uelewa juu ya athari za uharibifu wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema hayo katika ufunguzi wa Kongamano la vijana la Youth Change Summit linalojadili mada mbalimbali za mabadiliko ya tabia nchi lililo fanyika kwa siku mbili wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo amesema ni wakati wa vijana wasomi kuipeleka elimu hiyo maeneo ambayo hayafikiki kirahisi ili kujenga uelewa juu ya athari na madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira.
Katika hotuba yake pia Mh.Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa majiko banifu ambayo yanasaidia kupunguza au kuondosha kabisa vitendo vya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa sambamba na kuhamasisha matumizi ya mkaa mbadala.
Katika hatua nyingine amebainisha Serikali inaendelea na utaratibu wa kupunguza Kodi Katika nishati mbadala ili wananchi waweze kustahimili kwa kila kaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Youth PeaceMakeres Tanzania Mch. Godfrey Tahona Walalaze amesema wamelenga kufanya Kongamano hili la Mazingira kwa kulenga Mabadiliko ya tabia Nchi kwakuwa linaathiri maisha ya binadamu kwa ujumla na wakiamini vijana wanauwezo mzuri wa kubuni njia bora za kukabiliana na chanzo na athari ya Mabadiliko ya Tabia Nchi kwa maisha ya Sasa na baadae.