YPM Yaendelea Kutoa Mafunzo kwa Walimu Kuhusu Mfumo Mpya wa Midahalo wa Parliament Debate Format (PDF)

Katika kuhakikisha walimu wa shule za sekondari wanapata uelewa zaidi juu ya mfumo mpya wa uendeshaji wa midahalo ujulikanao kama Parliament Debate Format (PDF), Youth Peacemakers Tanzania (YPM) inaendelea kutoa mafunzo maalum kwa walimu kutoka shule mbalimbali za sekondari katika Wilaya ya Lushoto. Lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha wanafunzi wanatumia mfumo huu unaolenga kuwajengea uwezo wa kujenga hoja, kutetea mada, na kukuza ujasiri wa kuzungumza mbele ya hadhira.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na walimu kutoka shule za sekondari za Shambalai, Prince Claus, Magamba, Shekilindi, Kitala, Kwembago, Gologolo, Lushoto, Ubiri, Mlongwema na Migambo, pamoja na mwakilishi wa Mwenyekiti wa Maafisa Elimu Kata za Wilaya ya Lushoto, Bw. Valentino M. Hizza.

Baada ya mafunzo hayo, walimu kwa kushirikiana na YPM wameandaa ratiba maalum ya mashindano ya midahalo (debates) kwa wanafunzi, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mfumo huo mpya wa PDF. Kupitia ratiba hiyo, wanafunzi watapata fursa ya kutumia ujuzi waliopata darasani katika mijadala ya kitaaluma na kijamii, ikiwemo kujifunza kuheshimu mitazamo tofauti na kujenga hoja zenye mashiko.

YPM inaamini kuwa mfumo huu wa Parliament Debate Format (PDF) utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha uwezo wa wanafunzi wa kufikiri kwa kina, kujieleza kwa ufasaha, na kushiriki kikamilifu katika mijadala yenye tija kwa maendeleo yao na jamii kwa ujumla.


























