YPM Yaendesha Mafunzo ya Public Debate Format (PDF) kwa Walimu na Wakuu wa Shule Lushoto

Youth Peacemakers Tanzania (YPM), kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Wakuu wa shule na Walimu wa midahalo (debate) kutoka shule mbalimbali za sekondari wilayani Lushoto, wameendesha mafunzo maalum ya Uendeshaji wa Midahalo kwa njia ya kisasa inayojulikana kama Public Debate Format (PDF).

Mafunzo haya yamehusisha shule za Shambalai, Mlongwema, Ngulwi, Prince Claus, Magamba, Ubiri, Lushoto, Kitala, Kwemashai, pamoja na Migambo. Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo walimu na viongozi wa shule ili waweze kuwawezesha wanafunzi wao kushiriki mijadala ya kitaaluma kwa namna yenye tija, uhuru wa hoja, nidhamu ya kisomi, na uwezo wa kupambanua changamoto za kijamii na kitaifa kwa kutumia hoja zenye ushahidi.

Kupitia Public Debate Format (PDF), YPM inalenga kuimarisha ujuzi wa vijana katika mawasiliano, uongozi, kufikiri kwa kina, na kushiriki katika mijadala ya kisera. Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhamasisha ushiriki wa vijana katika utengamano wa jamii, utatuzi wa migogoro, na kukuza demokrasia shuleni.

YPM inaamini kuwa uwekezaji katika midahalo ni uwekezaji katika kizazi cha viongozi wa kesho — vijana wanaoweza kueleza, kusikiliza, na kushawishi kwa njia ya amani na mantiki.