Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika eneo la Manolo, Wilaya ya Lushoto, yamebeba ujumbe mzito wa kuwajibika katika uhifadhi wa mazingira kupitia kaulimbiu isemayo “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto aliyewakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Bi. Ikupa Mwasyoge. Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wanafunzi kutoka Shule za Sekondari Nywelo na Shume, vikundi vya afya na mazingira, wananchi, wadau wa mazingira pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali za mitaa.
Kwa kipindi cha tarehe 2 hadi 5 Juni, shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwa ni sehemu ya Wiki ya Mazingira. Tarehe 3 Juni wananchi walishiriki zoezi la usafi katika maeneo ya Maguzoni na Halmashauri, huku tarehe 4 Juni elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi ikitolewa kwa wananchi na washiriki mbalimbali.
Kilele cha maadhimisho kilifanyika tarehe 5 Juni ambapo shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo gwaride, igizo lenye ujumbe wa utunzaji wa mazingira, upandaji wa miti, usomaji wa risala pamoja na hotuba kutoka kwa viongozi mbalimbali.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Bi. Ikupa Mwasyoge alipongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri, vikundi vya mazingira, wadau pamoja na wananchi katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi.
“Jukumu la kutunza mazingira ni la kila mwananchi. Ni muhimu kuendelea kuzingatia kauli mbiu ya ‘Kata mti, panda mti’ ili kuhakikisha tunalinda mazingira yetu kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Bi. Ikupa.
Aidha, aliwataka wakulima na wafugaji kulinda vyanzo vya maji kwa kuepuka shughuli zinazoweza kuharibu mazingira, huku akisisitiza kuwa kila Halmashauri inapaswa kuhakikisha inapanda miti milioni 1.5 kama sehemu ya juhudi za kitaifa za uhifadhi wa mazingira.

