YPM na iTF Waadhimisha Siku ya Hedhi Duniani kwa Kuwakutanisha Wanafunzi wa Lushoto

Katika kuadhimisha Siku ya Hedhi Duniani, Youth Peacemakers Tanzania (YPM) kwa kushirikiana na Improving Tanzania Foundation (iTF) wameandaa maadhimisho maalum yaliyowakutanisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Wilaya ya Lushoto. Shule zilizoshiriki ni pamoja na Shambalai, Prince Claus, Lushoto, Kwembago, Gologolo, Shekilindi, Ubiri, Ngulwi na Kitala.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mwalimu Rashid Mswaki aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha vijana wanapata elimu sahihi kuhusu hedhi salama ili kuondoa unyanyapaa na dhana potofu zinazowakwamisha wasichana wengi kufikia ndoto zao.

“Hedhi si jambo la aibu bali ni sehemu ya maisha ya kila mwanamke na msichana. Elimu sahihi ndiyo njia ya kujenga jamii yenye uelewa na usawa,” alisema Mwalimu Rashid Mswaki.
Aidha, Inspekta Karim Celestine, Afisa wa Dawati la Jinsia Lushoto, alizungumzia masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kuyaunganisha na changamoto zinazowakabili wasichana kipindi cha hedhi. Alisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kulinda haki na usalama wa watoto wa kike shuleni na nyumbani.

Kwa upande wake, Madam Grace kutoka iTF alitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya pedi za kufua, namna ya kuzitumia kwa usalama pamoja na aina mbalimbali za pads zinazopatikana kwa matumizi ya wasichana.
Maadhimisho hayo yalitoa pia nafasi kwa wanafunzi kushiriki katika mjadala wa panel uliowakutanisha wawakilishi kutoka kila shule pamoja na mwanafunzi mmoja wa kiume. Kupitia mjadala huo, wanafunzi walizungumzia dhana potofu kuhusu hedhi na kusisitiza kuwa elimu ya hedhi si kwa wasichana pekee bali ni haki ya wavulana kujifunza pia ili kujenga jamii yenye uelewa, heshima na ushirikiano.

“Hedhi ni jambo la kawaida, hivyo wavulana pia wanapaswa kuelimishwa ili wawe sehemu ya kuondoa unyanyapaa na kuwapa wasichana mazingira salama na yenye kuelewana,” alisema mmoja wa washiriki wa panel.
Maadhimisho hayo yameendelea kuonyesha umuhimu wa ushirikishwaji wa vijana katika kujenga jamii yenye uelewa wa afya ya hedhi, usawa wa kijinsia na haki za mtoto wa kike. Kupitia ushirikiano kati ya YPM na iTF, vijana wameendelea kupata nafasi ya kujifunza, kushiriki na kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika jamii zao.


